DCI: Tunawatafuta wahalifu waliopora mali na kuwaibia Wakenya

Tom Mathinji
1 Min Read

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, (DCI) imesema imewatuma maafisa wake kuwatafuta wahuni walionakiliwa kwenye kanda za video, wakiwaibia Wakenya na kupora mali wakati wa maandamano dhidi ya serikali jana Jumanne.

Hatua hiyo ya DCI inajiri baada ya wahalifu kunakiliwa katika kanda za video wakiwaibia watu wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na vijana wa kizazi cha Gen Z kuwaomboleza wenzao waliofariki wakati wa maandamano ya amani.

Kupitia kwa taarifa katika mtandao wa X, idara hiyo iliwaonya wale wanaochukua fursa ya maandamano hayo kutekeleza uhalifu kuwa chuma chao ki motoni.

“DCI imewatuma maafisa kuwatafuta wahalifu walionakiliwa wakipora mali na wakiwaibia Wakenya barabarani, huku wakichukua fursa ya maandamano yaliyokuwa yakiendelea,” ilisema DCI katika taarifa.

Maandamano ya vijana dhidi ya serikali yaliingia wiki ya tatu jana Jumanne katika miji kadhaa mikuu kote nchini.

Jijini Nairobi, polisi walitumia vitoza machozi kuwatawanya waandamanaji ambao walikuwa wamekusanyika katika barabara kadhaa kuu katikati ya jiji.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *