Jimbo kuu la Nairobi la kanisa Katoliki limefafanua kuhusu ushiriki wa Kadinali John Njue katika kikao cha uteuzi wa Papa mpya kufuatia kifo cha hivi maajuzi cha Papa Francis.
Katika taarifa rasmi ya leo Mei 6, 2025, Askofu mkuu wa jimbo kuu la Nairobi Philip A. Anyolo alielezea kwamba Kadinali Njue hatashiriki shughuli hiyo muhimu kwa kanisa Katoliki ulimwenguni.
Huku akijibu maswali mengi yaliyosheheni ya ushiriki wa Kadinali Njue, Askofu Mkuu Anyolo alisema Kadinali Njue hatoweza kushiriki kutokana na hali yake ya afya.
“Ninathibitisha hapa kwamba hata ingawa Kadinali Njue anahitimu kuhusika katika kikao cha uteuzi wa Papa mpya na alialikwa rasmi na Nuncio wa Kenya, afisi ya Askofu Mkuu wa Nairobi iliarifu afisi kuu kwamba hatoweza kuhudhuria.” alisema Anyolo katika taarifa.
Kulingana na Anyolo, hali ya afya ya Kadinali Njue haitamruhusu kusafiri hadi Roma kwa ajili ya kikao hicho muhimu kinachopangiwa kuanza Mei 7, 2025 huko Vatican.
“Makadinali wanapojiandaa kuingia kikao hicho kesho, ninawasihi waumini wote waombe kwamba roho mtakatifu awaongoze wanapotekeleza jukumu lao muhimu la kuteua baba mtakatifu atakayeongoza kanisa letu.” aliandika Anyolo.
Askofu mkuu Anyolo pia aliwataka waumini wamwombee Kadinali Njue ili afya yake iweze kuimarika.
Maswali yamekuwa mengi kuhusu iwapo Kenya ingehusika katika uteuzi wa Papa mpya ambapo awali ilidaiwa kwamba Kadinali Nje amezidi umri wa miaka 80 na hivyo hawezi kushiriki.
Baadaye ilibainika kwamba bado hajatimiza umri huo lakini amekwazika kutokana na sababu za kiafya.
Makadinali watakaa kwenye kikao hicho hadi pale ambapo watachagua Papa shughuli ambayo huenda ikachukua saa chache, siku moja au hata siku kadhaa.