Davido ajivunia mafanikio ingawa hajashinda Grammy

Baada ya kuteuliwa mara tatu kuwania tuzo za Grammy, Davido sasa anaangazia mtindo wa kiasili kwa ajili ya mashabiki wa nyumbani.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki wa Nigeria, Davido, amefunguka kuhusu hisia zake kuelekea tuzo za Grammy baada ya kukosa kushinda mara tatu, huku pia akisimulia kuhusu hatua inayofuata katika taaluma yake.

Davido alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alitafakari safari yake katika tasnia ya muziki na kueleza kuridhika na mafanikio aliyopata hadi sasa.

Davido alibainisha kuwa ameafikia mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kutumbuiza katika majukwaa ya kimataifa, kujaza kumbi kubwa na kupata teuzi kadhaa za tuzo za Grammy katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Licha ya kutoshinda, aliweka wazi kuwa anajivunia mafanikio yake.

Kulingana naye, sasa anaelekeza nguvu zake mbali na kutafuta uthibitisho wa kimataifa na zaidi kuelekea kukumbatia asili yake.

Mwimbaji huyo alisema hatua inayofuata katika muziki wake itajikita zaidi katika sauti za Kiafrika, badala ya kuchanganya mitindo ili kuwavutia wasikilizaji wa Magharibi.

“Katika sehemu hii ya taaluma yangu, nimetumbuiza kila mahali, nimejaza kila ukumbi mkubwa, nimehudhuria tuzo tatu za Grammy katika miaka mitatu iliyopita,” alisema.

Nyota huyo aliendelea kusema kwamba muziki unaokuja sasa ni wa Davido halisi, ni wa Kiafrika sana.

Davido pia alizungumzia mashabiki wake wengi nchini Afrika Kusini, akifichua kuwa asilimia kubwa ya watu huko wanafahamu na kuunga mkono muziki wake.

Kwa miaka mingi, ameshirikiana na wasanii kadhaa wa Afrika Kusini na kupata vyeti mbalimbali vya mafanikio nchini humo.

Share This Article