David McCallum afariki akiwa na umri wa miaka 90

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji wa Marekani David McCallum, ambaye anafahamika sana kutokana na jukumu lake la uigizaji kama Daktari Donald ‘Ducky’ Mallard katika kipindi cha NCIS, ameaga dunia.

David aliaga Jumatatu Septemba 25, 2023 katika hospitali ya Presbyterian jijini New York kutokana na kile kilichotajwa kuwa sababu za kiasili.

Kampuni ya utangazaji ya CBS ambayo ilikuwa inapeperusha kipindi cha NCIS ndiyo ilitangaza kifo cha David ikimtaja kuwa mwigizaji na mwandishi aliyekuwa na talanta ya kipekee na ambaye alipendwa na wengi ulimwenguni.

CBS inasema mwigizaji huyo atakumbukwa milele kutokana na kazi zake za uigizaji.

Aliigiza kwenye makala zaidi ya 400 ya kipindi cha NCIS na kipindi cha miaka ya 1960 kwa jina “The Man from U.N.C.L.E.” ambavyo vilisababisha ateuliwe kuwania tuzo za Emmy na Golden Globes.

Kando na vipindi vya runinga mzee huyo aliigiza kwenye filamu kama “The Great Escape”, “A Night to Remember”, “Mosquito Squadron”, “Freud” na “The Greatest Story Ever Told”.

David ameacha mke wa umri wa miaka 56, watoto watatu wa kiume, mmoja wa kike na wajukuu wanane.

Kampuni ya CBS inapanga kumuenzi kwa njia ya kipekee itakaposherehekea miaka 20 ya kipindi cha NCIS.

Share This Article