Shughuli za uchukuzi katika barabara kuu ya Mombasa-Malindi, zimesambaratishwa baada ya daraja la Mbogolo kusombwa na mafuriko Jumamosi asubuhi.
Sehemu ya barabara hiyo upande wa Mombasa pia imeharaibiwa na mafuriko hayo.
Halmashauri ya kitaifa ya barabara kuu hapa nchini KeNHA, imewashauri wenye magari kutumia barabara ya Mombasa-Mazeras-Kaloleni-Mavueni-Kilifi, ikisema kuwa maafisa wake wanafanya kila juhudi kuirekebisha sehemu ya barabara hiyo.
“Daraja jipya linalengwa katika eneo hilo kama sehemu ya mradi wa barabara wa Kwa Kadzengo-Kilifi. Maafisa wa KeNHA wako katika eneo hilo kusaidia katika shughuli za uchukuzi. Madereva wanashauriwa kuepuka eneo hilo huku juhudi zikifanywa za kurejesha hali ya kawaida,” ilisema halmashauri hiyo kupitia ukurasa wake wa X.
Wakati huo huo uchukuzi umetatizwa katika eneo la Sultan Hamud, kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa kufwatia kufurika kwa Mto Sultan.