Wakazi wa vijiji vya Mbuyu na Ndururi katika eneo bunge la Ndaragwa, kaunti ya Nyandarua, wamelalamikia hali mbaya ya daraja linalounganisha maeneo hayo, ambalo linahatarisha maisha yao.
Kulingana na wakazi hao, iwapo utatumia daraja hilo lililojengwa enzi za ukoloni, huna budi kubebwa mgongoni ikiwa huna ujasiri wa kuhatarisha maisha yako kulivuka bila usaidizi.
Vijiji hivyo viwili vinavyopakana na wadi za Leshau Pondo na Central mtawalia, vinatumia kwa pamoja daraja hilo almaarufu Kanyagia.
Wakazi waliozungumza na shirika la habari la KBC, walielezea kustajabishwa kwao kutokana na hali mbovu ya daraja hilo, huku wakihoji jukumu la viongozi wa eneo hilo kushughulikia mahitaji ya jamii.
Licha ya ahadi nyingi zilizotolewa, wakazi hao hawajashuhudia maendeleo yoyote ya kuimarisha miundomsingi baada ya miaka kadhaa tangu nchi hii ijinyakulie uhuru.
Wakazi hao sasa wametoa wito wa kukarabatiwa kwa daraja hilo, ambalo linazidi kuhatarisha maisha yao kila uchao.