Bunge la Afrika Kusini limemchagua tena Cyril Ramaphosa kuwa Rais wa taifa hilo kufuatia mkataba madhubuti wa kubuni serikali ya muungano kati ya chama tawala cha ANC, na vyama vya upinzani.
Serikali mpya ya muungano inajumwisha chama cha ANC cha Ramaphosa, kile cha Democratic Alliance (DA) pamoja na vyama vingine vidogo.
Katika hotuba yake ya ushindi, Ramaphosa alipongeza muungano huo mpya, ambapo alisema wapiga kura wanawatarajia viongozi kuwahudumia na kushirikiana kwa manufaa ya kila mwananchi wa Afrika Kusini.
Mkataba huo uliafikiwa siku ambayo kulishuhudiwa vurumai ya juu ya kisiasa ambayo iliifanya bunge la kitaifa nchini humo kuandaa kikao hadi usiku ili kuthibitisha ni nani angechukua mamlaka katika utawala huo mpya.
Mkataba huo uliafikiwa kufuatia majuma kadhaa ya uvumi kuhusu chama ambacho chama cha ANC kingeshirikiana nacho baada ya kupoteza viti vyake vingi bungeni kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, kwenye uchaguzi uliaondaliwa mwezi uliopita.
Chama hicho kilipata asilimia-40 ya kura huku kile cha DA kikiibuka cha pili na asilimia-22.
Chama cha ANC awali kilikuwa kikipata zaidi ya asilimia-50 ya kura tangu taifa hilo liandae uchaguzi wake wa kidemokrasia mwaka-1994, uliomwezesha Nelson Mandela kuwa rais.