CUE yaonya kuhusu utoaji wa shahada wa taasisi ambayo haijaidhinishwa ya Northwestern Christian University

Onyo hili linafuatia kuibuka kwa habari kwamba mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alitunukiwa shahadha ya heshima ya uzamivu na chuo hicho.

Marion Bosire
2 Min Read

Tume ya elimu ya vyuo vikuu nchini -CUE imetahadharisha umma kuhusu shahada za heshima za uzamivu zinazodaiwa kutolewa na taasisi ya Northwestern Christian University, ambayo haijaidhinishwa.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, CUE ilisisitiza kwamba chuo hicho kikuu kinachoendesha shughuli zake nchini Kenya hakitambuliwi na tume hiyo na hakina idhini ya kutoa elimu ya chuo kikuu au kugawa hati za elimu ya juu.

Tume hiyo ya elimu ya vyuo vikuu nchini ilitangaza kutosajiliwa kwa taasisi hiyo kwa mara ya kwanza katika tangazo la gazeti Juni 2023, ambapo ilitahadharisha umma kwamba uhitimu wa chuo hicho hautatambuliwa humu nchini.

Tume hiyo ambayo ndiyo taasisi ya pekee ya serikali iliyotwikwa jukumu la kudhibiti elimu ya vyuo vikuu nchini kulingana na sura ya 210 ya sheria ya vyuo vikuu nchini inasisitiza kwamba utoaji wa hati za shahada bila idhinisho rasmi ni ukiukaji wa kanuni za kitaifa.

CUE imeanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo na imeahidi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya taasisi hiyo iwapo itahitajika kufanya hivyo.

Ushauri wa CUE kwa umma ni kuhakiki uidhinishaji wa vyuo vikuu na mipango mingine ya utoaji wa elimu ya juu nchini kupitia tovuti yake au kwa kufika kwenye afisi zake.

Tume hiyo imejitolea kuhakikisha kwamba ubora na uaminifu unadumishwa katika utoaji wa elimu ya juu nchini huku ikitunza viwango vya uhitimu wa kimasomo unaotolewa na taasisi zilizoidhinishwa.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *