Mabingwa mara 12 wa soka ya kitaifa ya wavulana baina ya shule za upili, Kakamega, waliwakwatua mahasimu wa jadi Musingu almaarufu Scorpion magoli mawili kwa yai katika fainali ya mashindano ya Magharibi.
Mchuano huo uliokuwa na hisia mseto na halaiki ya mashabiki wakiwemo Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na Gavana wa kaunti ya Bungoma Ken Lusaka, ulisakatwa ugani Kanduyi mjini Bungoma.
Mabao hayo yalitingwa na beki Fidel Odhiambo na kiungo Daniel Ombati katika kipindi cha pili cha muda wa ziada.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa muda wa miaka minne ambayo timu hizo zimechuana.
Kakamega watashiriki mashindano ya kitaifa kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa miaka sita.
Mara ya mwisho kucheza kiwango hicho ilikuwa mwaka wa 2018, ambapo ilinyakua taji hilo chini ya mwalimu na kocha mzoefu Brendan Mwinamo ambaye alihamia Musingu.
Mwaka wa 2020 na 2021, mashindano hayo hayakuandaliwa kwa sababu ya janga la ugonjwa wa korona.
Wengine waliokata kiu ya muda mrefu ni vipusa wa Archbishop Njenga waliowalaza mabingwa watetezi wa kitaifa, Butere magoli mawili kwa moja.
Kwenye voliboli, mabingwa mara tano wa kitaifa Malava na vidosho wa Mwitoti walijikatia tiketi ya kitaifa kwa ushindi wa seti tatu kwa mbili dhidi ya Butula, na seti tatu kwa nunge dhidi ya mabingwa mara 23 wa kitaifa, Lugulu mtawalia.
Mashindano ya kitaifa yatandaliwa mjini Thika kuanzia tarehe 26 mwezi huu na timu zitakazotia fora zitaenda mjini Morogoro, Tanzania kwa mashindano ya Afrika Mashariki.
Taarifa ya Boniface Musotsi