Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC ukipenda Leopards walipoteza nafasi chungu tele huku wakitoka sare ya bao moja na Chipolopolo ya Zambia katika mchuano wa ufunguzi wa kundi F katika kipute cha AFCON.
Mchuano huo ulipigwa Jumatano usiku katika uchanjaa wa Laurent Pokou mjini San Pedro nchini Ivory Coast.
Chipolopolo walikuwa wa kwanza kufumania lango la Chui wa DR Congo kupitia kwa Kings Kangwa, wakitumia makosa yaliyofanywa na mabeki.
Hata hivyo, sherehe hizo hazikudumu baada ya Chui kusawazisha katika kipindi hicho cha kwanza Yoane Wisa akiunganisha pasi ya Cedeic Bakambu.
DR Congo walibuni nafasi nyingi lakini washambulizi butu wakakosa kumakinika na kuwalazimu Zambia kujihami kwa zaidi ya dakika 60 za mchezo kunusuru pointi 1.
Morocco walioicharaza Tanzania mabao matatu kwa bila katika mechi ya awali, wanaongoza kundi hilo kwa alama tatu wakifutwa na Zambia na DR Congo kwa pointi 1 kila moja.