Mwanamuziki Chris Brown aliruhusiwa kurejea Marekani, huku akisubiri kuendelea kwa kesi inayomkabili ya shambulio kwa chupa katika klabu ya usiku mjini London mwaka 2023.
Jaji Tony Baumgartner aliruhusu mabadiliko ya masharti ya dhamana ya mwanamuziki huyo wa Marekani katika Mahakama ya Southwark Crown siku ya Jumanne.
Brown amekana mashtaka ya kushambulia na kusababisha majeraha ya mwili kwa Abraham Diaw katika eneo la Tape, klabu binafsi ya wanachama iliyoko Hanover Square, Mayfair, mnamo Februari 19, 2023.
Mwanamuziki huyo wa mtindo wa R&B wa umri wa miaka 36 pia amekana kosa la kuwa na silaha hatari hususan chupa katika eneo la umma na jaribio la kusababisha majeraha makubwa ya mwili.
Heidi Stonecliffe KC ambaye ni mwendesha mashtaka, alisema kuwa masharti ya dhamana bado yapo na ni mengi. Ada ya usalama ya pauni milioni 5 ambayo Brown aliamriwa kulipa kwa mahakama bado inabaki kuwa halali.
Mshitakiwa mwenza wa Brown, raia wa Marekani Omololu Akinlolu, wa umri wa miaka 39, pia amekana shtaka la kushambulia na kusababisha majeraha ya mwili.
Masharti ya awali ya dhamana ya Brown yaliruhusu aendelee na ziara yake ya muziki ya Uingereza kama ilivyopangwa.
Alitakiwa kuishi katika makazi maalum ambayo anwani yake inajulikana na mahakama. Hakuruhusiwa kuzuru klabu ambayo ni eneo la tukio husika la mwaka 2023, kuwasiliana na Diaw aliyemshtaki au kuomba hati za kusafiria za kimataifa.
Akitoa ruhusa kwa washtakiwa wote wawili kurejea Marekani, Jaji Baumgartner alisema siku ya Ijumaa kwamba watalazimika kurejea Uingereza watakapotakiwa kufanya hivyo.
Aliwakumbusha kuwa kukosa kufika mahakamani watakapohitajika kunaweza kuhatarisha dhamana zao.
Washtakiwa walithibitisha utambulisho wao na kukiri kwamba wanaelewa masharti mapya. Watafika tena katika mahakama hiyo mnamo Januari 28.
