Mchekeshaji maarufu nchini Vincent Mwasia maarufu kama Chipukeezy amejibu wakosoaji wake kwenye mitandao ya kijamii akisema yeye hawezi kuitiwa kazi akose kufanya.
Baadhi ya wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii walimtupia maneno makali pale alipochapisha picha za sherehe za mashujaa katika kaunti ya Kwale.
Watu hao walimwambia kwamba hafai kuchapisha picha kama hizo kwani ni kuunga mkono serikali ambayo wanahisi inawanyanyasa.
Kwenye ujumbe wa video Mwasia alisisitiza kwamba kazi ni kazi na hafai kuchukiwa kwa kazi anayofanya ili kujipatia riziki.
Alishangaa ni vipi anaweza kuitiwa kazi akatae ati kwa sababu watu wanataka kubadilisha Kenya. “Nyinyi kama kuna mpango wenu mmetengeneza mnataka kubadilisha nchi, ninawatakia kila la kheri.” alisema Chipukeezy.
Katika ujumbe mwingine wa video, mchekeshaji huyo alilalamika akisema sasa wafuasi hao wanamrejelea kama Mutuse, yule mbunge aliyewasilisha hoja ya kumbandua mamlakani naibu Rais.
Aliendelea kushangaa ni kwa nini hawataki afanye kazi na Rais William Ruto ilhali Rais sasa anashirikiana na mpinzani wake mkuu wa kisiasa Raila Odinga.
Msanii huyo alihimiza wakosoaji wake watengeneze nchi yenye umoja na wala sio chuki, Kenya ambayo ina nafasi ya kila mmoja hata wale ambao hawakubaliani nao kimawazo.
“Mimi ninawatambua mbaya, lakini ni lazima tukosoane kwa heshima.” alisema mchekeshaji huyo.
Wanaomuunga mkono kwa upande mwingine wanahisi kwamba yeye ni mwathiriwa wa mashambulizi ya mitandaoni huku wakimhimiza aendelee na maisha kama kawaida huku akisusia wakosoaji.