Kevin Chesang alishinda dhahabu ya kwanza ya Kenya, katika Makala ya 24 ya mashindano ya Riadha Afrika Jumatano usiku, jijini Accra,Ghana.
Chesang ,alinyakua dhahabu ya mita 10,000, jana usiku katika siku ya pili ya mashindano ,ikiwa dhahabu ya kwanza kwa Kenya ya mbio hizo tangu mwaka 2012 mjini Porto Novo,Benin.
Chesang aliye na umri wa miaka 20,aliibuka mshindi kwa muda wa dakika 28 sekunde 30.44.
Hagos Gared wa Ethiopia, alinyakua nishani za fedha huku Silas Senchura wa Kenya, akiridhia shaba.

Awali jana Edwin Too, alishinda fedha katika shindano la Decathlon, akiboresha shaba aliyoshinda mwaka 2024 nchini Cameron.
Kenya ilifunga siku ya pili kwa medali ya shaba ya mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti jinsia mchanyato.

Kenya ina medali nne kufikia sasa;dhahabu moja fedha 1 na shaba 2, huku mashindano hayo yakiingia siku ya nne leo Alhamisi Mei 14.
Fainali za Wakenya leo ni pamoja na mita 400 kwa wanaume na wanawake 800 kwa wanume na wanawake na mita 3,000 kuruka viunzi na maji wanaume.