Chebor na Kiprono washinda mbio za nyika za Machakos

Dismas Otuke
2 Min Read

Mauren Chebor na Asbel Kiprono, wameibuka mabingwa wa mbio za kilomita 10 za msururu wa kwanza wa mbio za nyika nchini ulioandaliwa leo katika chuo cha mafunzo ya walimu cha Machakos.

Chebor kutoka North Rift alikata utepe wa kwanza katika mbio za vipusa akitumia dakika 36 sekunde 22.9, akifuatwa na  Christine Njoki kwa dakika 36 sekunde 22.9, huku Esther Chemtai wa KDF akimaliza wa tatu kwa dakika 37 sekunde 13.7.

Sandrafelis Chebet wa Police na Winnie Cheptarus kutoka South Rift walimaliza katika nafasi za nne na tano mtawalia.

Kiprono,kutoka North Rift,alishinda mbio za kilomita 10 wanaume akitumia dakika 32 sekunde 11.2, akifuatwa kwa karibu na Francis Koumwa wa South Rift kwa muda wa dakika 32 sekunde 14.7.

Victor Kipruto wa North Rift alimaliza wa tatu kwa dakika 32 sekunde 29.1,akifuatwa na Edwin Bett na Naibei Kiplimo katika nafasi za 4 na 5 mtawalia.

Yvonne Chepchirchir wa Central Rift alishinda kitengo cha kilomita 6 wasichana akitumia dakika 21 sekunde 40.2, mbele ya Lonah Cherono na Florence Chepkoech, waliomaliza katika nafasi za pili na tatu mtawalia kwa dakika 21 sekunde 50.7 na dakika 21 sekunde 57.7 mtawalia.

Silas Senchura wa Ngong alishinda kilomita 8 kwa wavulana chini ya umri wa miaka 20 akiziparakasa kwa dakika 25 sekunde 27.4,akifuatwa na Simon Maywa na Clinton Kimutai katika nafasi za pili na tatu mtawalia.

Wanariadha na maafisa wa chama cha riadha Kenya walishiriki kwenye zoezi la upanzi wa miti kabla ya kaunza kwa mashindano.

Mbio za nyika kitakamilikia Kisii kwa mkondo wa 6 mapema Januari, kabla ya kupisha mashindano ya maeneo na yale ya kitaifa.

Share This Article