Makocha 12 wa Kenya walifuzu baada ya kuhitimu mafunzo mjini Miramas, Ufaransa, chini ya mpango wa ushirikiano baina ya Kenya na Ufaransa, katika sekta ya michezo.
Waliofuzu ni pamoja na makocha 9 wa riadha na wengine watatu wa Taekwondo, Uendeshaji baiskeli na wataalam wa tiba maungo.
Makocha hao walipitia mafunzo ya hali ya juu mjini Miramas, kuhusu mbinu za sasa na ukufunzi, teknolojia ya kisasa michezoni na vifaa na miundombinu ya kisasa michezoni .
Hafla hiyo ilihudhuriwa na waziri wa michezo na masuala ya vijana Salim Mvurya, aliyewapongeza makocha wa Kenya kwa ukakamavu na nidhamu ya hali ya juu .
Aidha Mvurya, alipongeza ushirikiano huo baina ya Kenya na Miramas na mchango wake maridhawa kukuza michezo humu nchini.
Waziri alihimiza haja ya kupanua ushirikiano huo hadi katika sekta za Sanaa, utamaduni na uchumi bunifu, ili kuwawezesha vijana kando na michezo.
Mvurya aliwaalika wadau wa Michezo kutoka ufaransa kuzuru Kenya, kubaini uwezekano wa ushirikiano katika kambi za mazoezi ya nyanda za juu eneo la Iten kaunti ya Elgeyo Marakwet .