Halmashauri ya mawasiliano nchini, CA imesema haina mipango ya kuzima huduma za intaneti siku ya Jumanne, Juni 25, 2024.
Kupitia kwa taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri hiyo David Mugonyi amesema wamepokea maswali mengi kuhusu madai ya kuvurugwa kwa huduma za intaneti.
“Halmashauri hii haina mipango yoyote ile ya kuzima intaneti au kuvuruga ubora wa uunganishaji,” alisema Mugonyi.
Amesema hatua hiyo itakuwa ukiukaji wa katiba, uhuru wa kujieleza na kanuni za halmashauri hiyo.
“Hatua hiyo itahujumu ukuaji wetu wa haraka wa uchumi wa dijitali, ambao unasaidia familia nyingi kote nchini,” alisema Mugonyi.
Hata hivyo, alitoa wito kwa Wakenya kutumia huduma za kidijitali kwa heshima na kwa mujibu wa sheria zilizopo.