Mamlaka ya Mawasiliano hapa nchini (CA), imekariri kujitolea kwake kuhakikisha uwepo wa mazingira bora kwa sekta ya utangazaji yanayoheshimu uhuru wa kutoa maoni na kujieleza.
Lydia Sitienei, ambaye ni Katibu wa mamlaka hiyo, amesema serikali inaunga mkono uhuru wa vyombo vya habari hapa nchini.
Kulingana na Sitienei, mamlaka hiyo inatambua jukumu muhimu linalotekelezwa na vyombo vya habari kwa ustawi wa taifa na imejitolea kuweka mazingira bora kwa vyombo vya habari hasa sekta ya utangazaji ili kuboresha demokrasia.
Aliyasema hayo jijini Mombasa wakati wa warsha ya kuwahamasisha wadau wa vyombo vya habari kanda ya pwani.
“Vile vile, vyombo vya habari vina wajibu wa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria. Suala hili ni muhimu katika kuhakikisha kuna nidhamu katika sekta hiyo,” alisema Sitienei.
Aliongeza kuwa mitandao ya kijamii imebadilisha mfumo wa utangazaji kwa kuwa mitandao hiyo imetumika kwa wingi kama majukwaa ya vyanzo vya habari.
“Majukwaa ya kijamii yameleta demokrasia katika vyombo vya habari na kusababisha ushirikiano na serikali, wanahabari, mashirika ya kijamii na wadhibiti.”