Bunge la kitaifa limeidhinisha hoja ya kufanya vikao vya ziada kwa wabunge kujadili hotuba ya Rais na shughuli za kuzingatiwa kabla ya mapumziko marefu ya mwezi Disemba.
Wabunge hao sasa watakuwa na vikao maalum Jumatatu, Jumanne, Alhamisi, na Ijumaa wiki ijayo, pamoja na siku tatu zaidi katika wiki ya kwanza ya Disemba.
Kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah aliyewasilisha hoja hiyo, alisisitiza haja ya marekebisho hayo ili kuepusha wabunge hao kutakiwa kurejea mapema kutoka mapumziko yao ya Krismasi , ambayo yataanza tarehe Disemba 6,2024 hadi Februari 10,2025 kuandaa vikao vya kushughulikia mijadala ambayo haijashughulikiwa.
“Tunataka kukamilisha shughuli zote zilizo mbele yetu kabla ya mapumziko marefu ya krismasi. Tunataka kutowaita wabunge wakati wa kipindi cha mapumziko hayo, huu ndio wakati pia wafanyakazi wetu wenye bidii watapumzika,” alisema Ichung’wah.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwapa wabunge muda wa kutosha kujadili hotuba ya Rais kwa taifa.
Rais William Ruto ameratibiwa kuhutubia kikao cha pamoja cha bunge siku ya Alhamisi, Novemba 21, 2024.
Zaidi ya hayo, wabunge wamepanga kuhudhuria michezo ya bunge la Afrika Mashariki (EALA) mjini Mombasa mnamo tarehe 6 Disemba.