Bunge la kaunti ya Kirinyaga limepitisha sheria ya kudhibiti utengenezaji na uuzaji wa pombe katika kaunti hiyo.
Wafanyabiashara ambao wanatengeneza, kusambaza au kuuza pombe bila leseni rasmi watashtakiwa na kufungwa kifungo kisichozidi miezi sita au kulipa faini takriban shilingi elfu 50.
Wauzaji rejareja wa pombe pia hawajasaazwa kwani watatumikia kifungo cha mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi elfu 100 au vyote kwa pamoja.
Uuzaji wa pombe kwa walio na umri chini ya miaka 18 umepigwa marufuku. Watakaopatikana na kosa hilo watafungwa miaka mitano au kulipa faini ya shilingi elfu 500.
Wanaouza pombe mita 300 kutoka makazi, taasisi za elimu na maeneo ya kuabudu nao watalipa faini ya shilingi elfu 100 au kufungwa miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Sheria hiyo imependekeza kuanzishwa kwa afisi ya mkurugenzi wa kudhibiti vileo ambayo itaongozwa na mkurugenzi ambaye ataajiriwa na Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti.
Mwenyekiti wa kamati ya jinsia na vijana Thomas Muriuki ambaye ni mwakilishi wa wadi ya mukure alisema ni hatua muhimu kwani sheria hiyo itadhibiti usambazaji wa pombe kali na kuondoa watengenezaji na wasambazaji wa kinywaji hicho hatari sokoni.
Mwakilishi wa wadi ya Kangai James Njiru Wambu ambapo zaidi ya watu 20 walifariki baada ya kunywa pombe haramu alisema hii itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa utumizi mbaya wa pombe katika eneo hilo.
Sheria hiyo inasubiri kutiwa sahihi na gavana wa kaunti hiyo Anne Waiguru ndani siku 14 zijazo.