Brussels Airlines yarejesha safari zake Nairobi

Kevin Karunjira
1 Min Read

Shirika la ndege la Brussels Airlines limerejesha safari zake za moja kwa moja jijini Nairobi baada kusitisha safari hizo kwa kipindi cha karibu mwongo mmoja uliopita.

Ndege ya shirika hilo ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA jana Jumatatu usiku.

Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini, KAA imetaja kurejeshwa kwa safari hizo kuwa mwanzo mpya wa kuunganisha bara la Ulaya na Afrika Mashariki.

Waliokuwepo kuilaki ndege hiyo wakati ikitua JKIA ni pamoja na Katibu katika Wizara ya Uchukuzi Mohamed Daghar, mwenzake wa Uhamiaji Prof. Julius Bitok na mwenyekiti wa bodi ya KAA Caleb Kositany.

Kositany akielezea mipango iliyowekwa ya kupanua uwanja wa JKIA ili kuongeza uwezo wa uwanja huo kushughulikia abiria wengi na ndege zaidi na hivyo kuifanya Nairobi kuwa kituo bora cha usafiri wa anga barani Afrika.

Kwa upande wake, Daghar alisema kurejeshwa kwa safari za Brussels Airlines ni ushuhuda tosha wa kufufuka kwa sekta ya usafiri wa anga kutokana na athari za janga la virusi vya korona.

Aliongeza kuwa serikali itatumia manufaa yaliyopatikana katika sekta ya uchukuzi kuimarisha sekta ya usafiri wa anga wakati ikiangazia kuimarisha uchumi.

 

 

 

 

Share This Article