Bodi ya mapato ya serikali ya kaunti ya Meru imepongeza hatua ya kuzinduliwa kwa eneo la viwanda katika kaunti hiyo.
Meneja mkuu wa bodi hiyo Bw.Francis Mugai amesema kama bodi wana matumaini kwamba mapato ya kaunti yataongezeka maradufu mara tu ujenzi wa eneo hilo la viwanda utakapokamilika na kuanza kutumika.
Waziri wa biashara na viwanda Moses Kuria alizindua ujenzi wa eneo la viwanda katika kaunti ya Meru Jumatatu.
Akizungumza katika afisi yake eneo la Makutano huko Meru, Mungai alisema ukaribu wa eneo hilo la viwanda la Meru na mpaka wa kaunti ya Isiolo na uwanja wa ndege wa Isiolo utachochea zaidi ongezeko la mapato.
Alisema pia kwamba kituo hicho cha viwanda kitachochea ukuaji wa biashara nyingine kama vile nyumba za kukodisha na hoteli na kuchangia mapato zaidi kwa kaunti kwani wamiliki wa biashara hizo watahitajika kuwa na leseni za kuhudumu kutoka kwa kaunti.
Mugai alisema eneo la viwanda katika kaunti ya Meru ni mradi muhimu kwa sababu utavutia kampuni kadhaa na hivyo kutoa nafasi za ajira kwa wenyeji.
Serikali ya kaunti ya Meru, imetenga shilingi milioni 250 za ujenzi wa eneo hilo la viwanda huku serikali kuu ikichangia kiasi sawa na hicho.