Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken leo Alhamisi amefanya mazungumzo nchini Qatar, ambayo ni mpatanishi mkuu katika vita eneo la Gaza.
Blinken anatafuta kuzidisha kasi ya kusitishwa kwa vita hivyo baada ya Israel kumuua kiongozi wa kundi la Hamas.
Baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem, Blinken alielekea Saudi Arabia na kisha Qatar, ambako atatafuta kutathmini msimamo wa Hamas kuhusiana na makubaliano ya kusitisha vita.
Blinken “alijadili juhudi mpya za kuhakikisha kuachiliwa kwa mateka na kumaliza vita katika eneo la Gaza” na emir wa taifa hilo la Ghuba, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, ilisema Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Kisha baadaye alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani, ambaye kwa pamoja watawahutubia wanahabari.
Hiyo ni ziara ya 11 ya Blinken katika eneo hilo tangu kundi a Hamas lililpofanya shambulizi nchini Israel Oktoba 7, 2023.
Hajaambulia chochote wakati wa ziara hizo.
Lakini chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi wa urais nchini Marekani, Rais Joe Biden amepata matumaini mapya baada ya Israel kumuua kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar katika Ukanda wa Gaza.