Bitok: Uchapishaji wa vitambulisho vipya kuharakishwa

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakenya kupokea vitambulisho vya taifa bila malipo.

Serikali imesema itakamilisha shughuli ya uchapishaji wa vitambulisho vipya vya kitaifa katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Katibu wa Idara ya Uhamiaji na Huduma kwa Wananchi Julius Bitok, amesema ucheleweshwaji wa shughuli hiyo umetokana na hitilafu za mashine ya kuchapisha stakabadhi hizo ambayo sasa imefanyiwa ukarabati, pamoja na kesi iliyowasilishwa mahakamani ya kusimamisha shughuli hiyo.

Kwa sasa, nakala 15,000 za vitambulisho hivyo al maarufu Maisha Card zinachapishwa kila siku huku nakala laki sita zikiwa tayari zimechapishwa.

“Nawahakikishia Wakenya kwamba mashini zetu sasa zinafanya kazi, na tutapata vitambulisho bila kuchelewa jinsi ilivyokuwa hapo awali,” alisema Bitok.

Katibu huyo aliwahakikishia Wakenya kwamba shughuli ya uchapishaji wa kadi hizo inaendelea saa 24 ili kumaliza mrundiko ulioko.

kulingana naye, takriban maombi 8,000 ya vitambulisho hupokelewa kila siku.

Serikali pia inatarajia kununua mashine nyingine mpya ya uchapishaji mwezi ujao.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article