Bima ya SHIF: Waziri Barasa ataka umma kuelimishwa

Martin Mwanje
2 Min Read

Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa ametoa wito wa kila jitihada kufanywa kwa udi na uvumba kuelimisha umma kuhusiana na Bima mpya ya Afya ya Jamii, SHIF. 

Bima hiyo itakayoanza kutekelezwa Oktoba 1 mwaka huu itachukua mahali pa Bima ya Afya ya Kitaifa ya NHIF.

Dkt. Barasa amesema licha ya juhudi kubwa walizofanya kama wizara kuelimisha umma kuhusiana na bima hiyo, ukosoaji wake mkubwa umetokana na kukosa kuelewa manufaa yake.

“Muhimu zaidi, ni lazima tuuelimishe umma juu ya wajibu wao na hasa ukweli kwamba wanahitaji kujisajili ili kupata huduma,” aliongeza Waziri huyo.

Aliyasema hayo wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya Wizara yake na ile ya Usalama wa Kitaifa juu ya kuzinduliwa kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA katika Shule ya Mafunzo ya Serikali, KSG leo Jumatano.

SHA itasimamia utekelezaji wa SHIF.

Wakati zikiwa zimesalia chini ya siku saba kabla ya kuzinduliwa kwa bima ya SHIF, Dkt. Barasa alitoa wito wa kila juhudi kufanywa kuhakikisha kila Mkenya anafahamu manufaa ya bima hiyo na kujisajili.

“Kwa wakati huu kipaumbele ni kuhakikisha kaya zinajisajili, zinatoa michango wakati zikijitayarisha kupokea huduma Oktoba mosi,” alisema Dkt Barasa.

“Tafadhali ihusishe jamii kupitia kwa wazee wa vijiji, machifu na wahudumu wa afya ya jamii kuhusiana na uzinduzi wa SHA,” aliongeza Waziri huyo aliyetaka ujumbe kuhusiana na uzinduzi huo kutolewa kupitia hafla mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazishi, harusi, matukio ya shule na kadhalika.

Alidokeza kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanasajili asilimia 60 ya kaya katika kila kaunti kufikia Oktoba 1.

Kwa upande wake, Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki aliahidi kuwa maafisa wa utawala wa serikali kuu (NGAOs) watakuwa mstari wa mbele katika usajili wa kaya milioni 12 kuelekea uzinduzi wa bima hiyo.

Prof. Kindiki alibainisha kuwa sheria zote zinazohitajika kwa utekelezaji wa bima hiyo zimewekwa kuhakikisha uzinduzi wake unafanywa bila kukumbana na vikwazo vya aina yoyote.

Hadi kufikia sasa, Wakenya wapatao milioni 1.6 wamejisajili kwa bima ya SHIF.

 

Share This Article