Biden amtaja Xi kuwa ‘Dikteta’ siku moja baada ya mazungumzo ya Beijing

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais wa Marekani Joe Biden .

Rais wa Marekani Joe Biden amemtaja Rais wa China Xi Jinping kuwa dikteta katika hafla ya kuchangisha fedha jijini California.

Matamshi yake yanakuja siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kukutana na Rais Xi kwa mazungumzo mjini Beijing, ambayo yalilenga kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu.

Rais Xi alisema baadhi ya mafanikio yamepatikana mjini Beijing huku Blinken akidokeza kwamba pande zote mbili ziko tayari kwa mazungumzo zaidi.

China bado haijajibu maoni ya Biden.

Rais Biden, katika hafla ya kuchangisha pesa Jumanne usiku kwa saa za huko, pia alisema Rais Xi alikuwa na aibu juu ya mvutano wa hivi maajuzi kuhusu puto ya kijasusi ya Uchina ambayo ililipuliwa juu ya Marekani.

Ziara ya Blinken mjini Beijing – ya kwanza kwa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani katika takriban miaka mitano – ilianzisha upya mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili.

Biden na Xi waliipongeza hatua hiyo kama nzuri. Lakini Blinken aliweka wazi kuwa tofauti kubwa zimesalia kati ya nchi hizo mbili.

Marekani na China zimekuwa zikitofautiana kwa muda mrefu kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo biashara, haki za binadamu na Taiwan.

Lakini mahusiano yamezorota hasa katika mwaka uliopita.

Website |  + posts
Share This Article