Benki ya Equity inalenga kuwekeza angalau asilia mbili ya mapato yake katika miradi endelevu katika masoko saba inakohudumu kwa sasa.
Kulingana na benki hiyo, mikopo kwa mashirika madogo na ya kati chini ya Mpango wa Young Africa Works ilifikia jumla ya shilingi bilioni 223.1 zilizotolewa kwa kampuni 246,701, hatua ambayo ilihamasisha ujasiriamali na kubuni nafasi milioni 1.2 za kazi.
Kadhalika, benki hiyo ilitoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 73.3 kusaidia wakulima na mashirika madogo na ya kati milioni 3.98 katika chakula na kilimo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti Endelevu ya Equity Group ya Mwaka 2022, Afisa Mkuu Mtendaji wa benki hiyo Dkt. James Mwangi alisema benki hiyo inawekeza pakubwa katika miradi endelevu na kutoa wito wa ushirikiano katika kuboresha usalama wa chakula, huduma za matibabu na elimu.
Ripoti hiyo inaangazia tofauti za malipo katika benki hiyo, ambapo inaashiria kuwa wanaume bado wanalipwa fedha zaidi kuliko wanawake wanaofanya kazi sawia nchini Kenya na Tanzania kwa asilimia 52 ikilinganishwa na nchi za DRC, Sudan Kusini, Rwanda na Uganda, suala ambalo linafuatiliwa kwa karibu kuhakikisha usawa wa malipo unaboreshwa katika benki hiyo.
Wazungumzaji wakati wa uzinduzi huo walitoa wito wa kuwepo ushirikiano na kaunti katika ufadhili wa mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi wa kaunti hizo.