Baraza la Vyombo vya Habari Nchini – MCK limelaani hatua ya maafisa wa polisi kujifanya kuwa wanahabari ambao wanaangazia matukio kwenye maandamano yanayoendelea huku nia yao ikiwa kuwakamata waandamanaji.
Kwenye taarifa, Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo David Omwoyo, alisema vitendo kama hivyo vinahatarisha maisha ya wanahabari wanapokuwa kazini. Alikitaja kitendo hicho kuwa ishara ya ukosefu wa nidhamu kwa upande wa polisi.
Taarifa yake Omwoyo inafuatia tukio lililonaswa na wanahabari ambapo afisa wa polisi ambaye alikuwa miongoni mwa wanahabari alikimbia na kumkamata mmoja wa waandamanaji na kukimbia naye hadi kwenye gari la maafisa wa polisi mtaani Mathare, Nairobi.
Huku akionyesha kuridhika na kuachiliwa huru kwa wanahabari waliokuwa wamekamatwa awali wakiangazia matukio kwenye maandamano, Omwoyo alisema hawakustahili kukamatwa.
Aliongeza kuwa kazi ya uanahabari imelindwa na vifungu nambari 33, 34 na 35 vya katiba ya Kenya.