Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kutaka “kusitisha mapigano mara moja” huko Gaza, baada ya Marekani kujiepusha kutumia kura yake ya turufu, kubadili msimamo wake wa awali.
Azimio hilo pia linataka kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote.
Baraza hilo lilikuwa limekwama tangu vita vianze mwezi Oktoba, na kushindwa mara kwa mara kukubaliana juu ya wito wa kusitisha mapigano.
Hatua hiyo ya Marekani inaashiria kuongezeka kwa tofauti kati yake na mshirika wake Israel kuhusiana na mashambulizi ya Israel huko Gaza
Washington imeikosoa Israel kutokana na kuongezeka kwa idadi ya vifo huko Gaza, ambapo zaidi ya watu 32,000 – hasa wanawake na watoto – wameuawa katika mashambulizi ya Israel, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Marekani pia imeishinikiza Israel kuhakikisha msaada unafikishwa Gaza, ambako inasema wakazi wote wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha uhaba wa chakula.
Umoja wa Mataifa umeishutumu Israel kwa kuzuia misaada; Israel imelaumu Umoja wa Mataifa, ikiishutumu kwa kushindwa kutekeleza usambazaji.