Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle wamemuunga mkono kwa kauli moja mgombea urais wa chama cha Democratic Kamala Harris.
Wakihutubia Kongamano la Kitaifa la chama hicho usiku wa Jumanne, wawili hao waliwahimiza wafuasi wa vyama vyote vya kisiasa nchini Marekani kujitokeza na kupiga kura kwa wingi ili kumshinda Donald Trump katika uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba.
“Matumaini yanarejea,” Bi. Obama aliuambia umati wa watu katika kongamano hilo mjini Chicago, akiashiria “Matumaini na mabadiliko” maneno ambayo yalikuwa kaulimbiu ya kampeni ya mume wake alipogombea urais.
Wafuasi hao mashuhuri zaidi wa Chama cha Democratic walimsifu Harris huku wakimkosoa mgombea wa urais wa Chama cha Republican Donald Trump – ambaye kwa mtazamo wao urais wake ulikumbwa na “machafuko na fujo”.
Barack na Michelle Obama pia walitoa wito kwa wafuasi wa chama cha Democratic kutopoteza mwelekeo na kwani siku zinayoyoma na wakiongeza kuwa mchuano dhidi ya Trump sio rahisi.
“Usifanye masiara, mchuano utakuwa mkali,” Obama alisema.
Walisisitiza kuwa uchaguzi wa Novemba utaamuliwa katika majimbo machache muhimu yenye ushindani mkali.
“Kazi yetu ni kuwashawishi watu kwamba demokrasia inaweza kuleta mafanikio,” alisema Barack Obama akiongeza kuwa “Kamala anaelewa hili.”
Michelle Obama kwa upande wake alisema kwamba Harris ni “mmoja wa watu wenye uwezo kuwahi kugombea wadhifa wa urais”.
“Na yeye ni mmoja wa watu wenye hadhi kubwa, kupigia kura ni heshima kwa mama yake, kwa mama yangu, na pengine kwa mama yako pia,” Bi Obama alisema.