Banky W aunga mkono kampeni ya wanawake kuwezeshwa kifedha

Marion Bosire
1 Min Read
Banky Wellington

Mwanamuziki wa Nigeria Banky Wellington ambaye sasa anaishi nchini Marekani na familia yake, ameunga mkono kampeni ya kuwezesha wanawake kifedha #HerMoneyHerPower.

Amechapisha video inayomwonyesha akitekeleza majukumu mbali mbali ya nyumbani kama vile kuosha vyombo, kufagia, kutunza mtoto na hata kupika.

Mume huyo wa mwigizaji Adesua Etomi anaelezea kwamba ndoa ni ushirikiano wa kiwango cha asilimia mia moja kwa kila mmoja na wala sio kugawana asilimia 50-50.

Mfano aliotoa wa ushirikiano ni kwamba alichukua majukumu yote ya nyumbani yanayojumuisha kutunza mwanao wa kwanza wa umri wa miaka mitatu huku mkewe akiwa mjamzito.

Anahisi kwamba kuunga mkono uhuru wa kiuchumi na kifedha kwa wanawake ni muhimu naye anafanya hivyo kwa kushughulika nyumbani.

Banky alisema anaendelea pia kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya usimamizi wa sera katika chuo cha Georgetown nchini Marekani na anaunga mkono ajira ya kina mama ulimwenguni kote.

“Tunapoinua wanawake, tunainua ulimwengu. Wanaume tafadhali tekeleza wajibu wenu.” alihimiza Banky W.

Kampeni ya #HerMoneyHerPower ilianzishwa na Bella Naija na lile la The She Tank kwa lengo la kuhimiza wanawake kupiga hatua katika kuafikia uhuru wa kifedha na kuchochea wanaume kuwaunga mkono.

Mwigizaji tajika Funke Akindele ndiye balozi wa kampeni hiyo.

Website |  + posts
Share This Article