Bandari ya Mombasa imepiga hatua kubwa katika kuimarisha shughuli zake licha ya hali ngumu ya kiuchumi duniani katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Kiwango cha mizigo inayopakuliwa na kupakiwa kwenye bandari hiyo kimeongezeka kwa asili mia 6.2.
Mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya bandari nchini kapteni William Ruto alisema bandari hiyo ilishughulikia makasha milioni 1.62 ya futi 20,hii ikiwa nyongeza ya asili mia 11.9.
Alisema hayo yalitokana na kushughulikiwa haraka kwa meli zinazotia nanga kwenye bandari hiyo hasa muda wa upakiaji na upakuaji wa mizigo.
Kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na meneja wa uhusiano mwema wa halmashauri hiyo Edward Kamau wakati wa mashindano ya gofu huko Kisumu, Ruto alisema kiwango cha mizigo inayopitia kwenye bandari hiyo kwenda na kutoka mataifa jirani kimeongezeka kwa asili mia 11.5.
Ingawaje Uganda ndio mteja mkubwa wa bandari hiyo,halmashauri hiyo pia imeshuhudia kuongezeka kwa biashara kutoka mataifa ya Sudan kusini na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Biashara katika bandari ya Kisumu pia imeimarika kwa kiwango cha asili mia 11.9 .