Babu owino asema kamwe hatasahau siku ya leo

Marion Bosire
2 Min Read

Mbunge wa eneo la Embakasi Mashariki katika kaunti ya Nairobi Paul Ongili Owino, maarufu kama Babu Owino, amesema kamwe hatasahau siku ya leo, siku ambayo kifo cha shujaa wake kilitokea.

Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Babu alimtaja marehemu Raila Odinga kuwa zaidi ya mshauri wake katika masuala ya kisiasa kwani alikuwa kama baba yake.

“Raila Amolo Odinga alikuwa zaidi ya mshauri wangu wa kisiasa, alikuwa kama babangu” aliandika Babu akiongeza kusema kwamba alikua bila baba kwani babake mzazi aliaga dunia akiwa darasa la tatu.

Anasema alipokuja Nairobi, alikutana na Baba Raila Odinga ambaye alimkaribisha na akawa babake katika siasa na katika maisha kwa jumla.

“Nilimpenda sana na kifo chake kimeacha shimo kubwa katika moyo wangu, shimo ambayo ni Mungu pekee anaweza kuijaza” aliendelea kusema Owino kwenye ujumbe wake wa kumwomboleza Baba.

Kiongozi huyo barubaru alitoa ujumbe wa pole kwa familia ya Raila ambapo alimtaja mjane Mama Ida, wanawe Rose Odinga, Junior Odinga, Winnie Odinga, wajukuu na jamii kwa jumla.

“Siwezi hata kuanza kuwaza kuhusu huzuni mliyo nayo. Ninaweza tu kuwaombea Mungu awape faraja na nguvu inayozidi uelewa wote wakati huu mgumu.” Alisema.

Babu hata hivyo alihimiza wananchi na haswa wafuasi wa Odinga, washerekee urithi wakeambao alisema kamwe hautafutika.

Website |  + posts
Share This Article