Mwili wa babake mwanamuziki David Kamoni Mathenge maarufu kama Nameless utazikwa Alhamisi Aprili 17, 2025, kulingana na tangazo kwenye gazeti.
Nameless alichapisha picha ya tangazo hilo na kulingana na maelezo, ndugu, jamaa na marafiki wamekuwa wakikutana nyumbani kwa mzee Joshua Solomon Mathenge huko Kiserian kila siku saa tisa hadi saa 11 jioni kwa ajili ya kupanga mazishi.
Mikutano mingine imekuwa ikifanyika katika kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi ambapo wa mwisho utaandaliwa kesho Jumanne Aprili 15, 2025 kati ya saa 11 unusu jioni na saa mbili usiku.
Ibada ya kumuenzi mzee Mathenge iliandaliwa nyumbani kwake huko Kiserian, jana Jumapili kuanzia saa nane mchana.
Mwili wake utaondolewa kwenye makafani ya Montezuma Monalisa Alhamisi Aprili 17, 2025 saa mbili asubuhi kwa ajili ya mazishi, hafla ambayo inatarajiwa kuanza saa nne unusu asubuhi siku hiyo hiyo.
Mzee aliaga dunia Aprili 6, 2025 baada ya kuugua na katika kutangaza kifo cha babake, Nameless alishukuru akisema, “Lala salama baba! Nimebarikiwa kupita kiasi kuwa nawe kama baba.”