Baba anatosha achaguliwe – Tanzania yamuunga mkono Raila

Marion Bosire
2 Min Read

Leo, Agosti 27, 2024, Rais wa Kenya William Samoei Ruto aliandaa hafla ya kuzindua rasmi uwaniaji wa Raila Odinga wa uenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika AUC.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa nchi mbali mbali za eneo la Afrika Mashariki akiwemo Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete na Rais wa sasa wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.

Alipopatiwa fursa ya kuzungumza, Kikwete alitangulia kufafanua kwamba yeye ni sehemu ya Ujumbe wa Tanzania na hotuba yao ingetolewa na Rais Samia. Hata hivyo alishukuru kwa mwaliko huku akimtakia Raila kila la Heri kwenye kinyang’anyiro hicho.

Jakaya alimpongeza kwa kuchaguliwa na Kenya kuwania wadhifa huo wa Afrika akiongeza kusema kwamba iwapo atafanikiwa kushinda, bara Afrika litapata kiongozi mzuri.

Zamu yake ilipowadia, Rais Samia alisema kwamba yeye hurejelewa kama “Mama” nchini Tanzania na amekuja kumuunga mkono “Baba” Raila Odinga anavyorejelewa na wakenya.

Samia alisema wakati wa kuzinduliwa kwa umoja wa Afrika mwaka 2002, watu wa bara hili walikumbushwa maazimio ya waanzilishi wa mataifa ya Afrika ambayo ni uhuru wa kisiasa, heshima ya kibinadamu na kujikomboa kiuchumi.

Kulingana naye maazimio hayo yanasalia kuwa msingi wa matamanio ya umoja wa Afrika.

Huku akisifia hatua kubwa zilizopigwa na umoja wa Afrika, Rais Samia alitaja hatua zilizosalia ambazo ni lazima zitekelezwe na kuhakikisha sauti ya Afrika inasikika ulimwenguni.

Rais Samia alidhihirisha imani kwamba Raila Odinga anaweza kuendeleza kazi iliyosalia katika umoja wa Afrika ndiposa Tanzania imeamua kumuunga mkono katika uwaniaji wake.

“Tanzania inasema, Baba anatosha achaguliwe.” ndivyo alivyokamilisha hotuba yake Rais Samia.

Website |  + posts
Share This Article