Baadhi ya wabunge kupinga Mswada wa Fedha nje ya bunge

Tom Mathinji
2 Min Read

Baadhi ya wabunge walioupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024, wamesema wataendelea  kuishinikiza serikali kutupilia mbali mswada huo.

Wakizungumza muda mfupi baada ya mswada huo kupita baada ya kusomwa kwa mara ya pili katika bunge la taifa, wabunge hao wengi wakitoka upande wa upinzani, walisema hawajashindwa vita dhidi ya kuangusha mswada huo.

“Tutapinga mswada huo bungeni na nje ya bunge. Tutawahimiza wakenya kuendelea na kushiriki maandamano ya amani. Tutahakikisha mssilahi ya wakenya yanapewa kipaumbele,” alisema mbunge wa Nyando Jared Okello.

Huku akisikitika kuwa baadhi ya wabunge wa upande wao walipiga kura kuunga mkono mswada huo, kiranja wa upande wa wachache katika bunge la taifa Junet Mohamed, alisema upinzani utatoa taarifa kuhusu swala hilo siku ya Ijumaa.

“Tungefanya vyema kama wabunge. Mswada huu si wa wakenya kutoka sehemu moja. wakati mswada unapitishwa bungeni ni wa wakenya wote,” alisema Junet.

Mbunge wa Mathare Anthony Oluoch, alilalamika kuwa mchakato wa kutoa maoni ya umma kuhusu mswada huo  ulikuwa ni hujuma.

“Nawahimiza Gen Z kuendeleza maandamano. Mapambano haya hayapaswi kukoma, tunawaunga mkono,” alisema Oluoch.

Aidha wabunge hao wa upinzai walisema watashinikiza vifungu vya mswada huo kufanyiwa marekebisho kuanzia wiki ijayo, ili kuondoa vipengee vinavyodhaniwa kuwa na utata.

Walitoa wito kwa polisi kukoma kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wanaopinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.

“Serikali inapaswa kufahamu kuwa watoto wa wabunge kutoka pande zote ndio wanaandamana. serikali inapaswa kuchukua hatua. Mambo hayaendi sawa hapa nchini,” alisema mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *