Mwanamuziki wa Nigeria Ayra Starr, amepata fursa ya kwanza ya kuigiza na anaanzia Hollywood ambayo ni ndoto ya waigizaji wengi ulimwenguni.
Binti huyo wa umri wa miaka 22 amejumuishwa kwenye kundi la watakaoigiza filamu ya riwaya ya ‘Children of Blood and Bone’ iliyoandikwa na Tomi Adeyemi.
Kitabu hicho kilizinduliwa rasmi mwaka 2018 baada ya kuandikwa kwa muda wa miezi 18 na mzaliwa huyo wa Nigeria ambaye pia ni raia wa Marekani Tomi Adeyemi.
Sasa kampuni ya uandaaji filamu ya Lucasfilm, iliyohusika katika kuandaa filamu kama “Star Wars”, imeamua kugeuza kitabu hicho kuwa filamu.
Filamu hiyo inahusisha waigizaji wengine wa Nigeria au Nollywood kama or Richard Mofe–Damijo, Pamilerin Ayodeji, Shamz Garuba, Temi Fagbenle, Zackary Momoh, Kola Bodunde na Saniyya Sidney.
Iko katika kiwango cha maandalizi na inatarajiwa kuzinduliwa mwaka 2027.
Nyota hao wa Nigeria watapata fursa ya kutagusana na waigizaji tajika ulimwenguni kama Cynthia Erivo, Viola Davis, Idris Elba na wengine.
Uhusika wa Ayra Starr kwenye filamu hiyo ni hatua kubwa maishani na inajiri baada yake kupokea tuzo ya muungano wa kampuni za kurekodi muziki nchini Marekani almaarufu RIAA.
Hii ni baada ya wimbo wake uitwao Santa kuuzwa zaidi ya mara milioni 10 nchini Marekani.