Awamu ya kwanza ya tamasha la maigizo ya ukumbini la Lagos kuandaliwa Novemba

Marion Bosire
2 Min Read

Tamasha la kimataifa la maigizo ya ukumbuni la Lagos litazinduliwa rasmi mwezi Novemba mwaka huu wa 2024 na linatizamiwa kukutanisha wadau wa sekta hiyo kutoka sehemu mbali mbali ulimwenguni.

Wakili Bolanle Austen-Peters ambaye hujihusisha na maandalizi na uelekezaji wa filamu na maigizo ya jukwaani ndiye mbunifu aliyekuja na wazo la tamasha hilo na anashirikiana na serikali ya jimbo la Lagos nchini Nigeria.

Akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo, Bolanle alisema kwamba tasnia ya ubunifu ni muhimu kwa nchi zote zinazostawi na Nigeria imebarikiwa na talanta mbali mbali.

“Ni muhimu kwetu kutoa jukwaa la wabunifu kuonyesha kazi zao, kutoa hadithi zetu na kuuza nje falsafa zetu pamoja na uadilifu.” alisema Bolanle.

Tamasha hilo litaandaliwa kati ya Novemba 15 na 17, 2024 katika kumbi kadhaa jijini Lagos kama vile ukumbi wa kitaifa uliopatiwa jina la Wole Soyinka, ukumbi wa Terra Kulture, ule wa Muson Centre pamoja na John Randle Centre.

Kila ukumbi utakuwa na maonyesho ya aina fulani ya kazi za ubunifu kama maigizo ya kimuziki, maigizo ya kawaida na mengine.

Bodi ya washauri ya tamasha hilo inajumuisha watu tajika katika tasnia ya ubunifu wakiwemo Joke Silva, Femi Elufowoju Jr, Chioma Ude, Jahman Anikulapo, Israel Eboh, Samuel Perry, Kehinde Bankole, Osas Ighodaro, John Momoh, Karl Toriola, Yemi Idowu, Ron Kunene, Ladi Chinede, Donald Duke na Yewande Zaccheus.

Watakaohudhuria watafaidika pia kutokana na mafunzo yatakayotolewa na wajuzi wa sekta hiyo kama njia ya kunoa makali yao.

Share This Article