Askofu Allan Kiuna wa kanisa la JCC amefariki

Tom Mathinji
2 Min Read
Askofu Allan Kiuna.

Askofu Allan Kiuna ambaye ni mwanzilishi wa kanisa la Jubilee Christian JCC, ameaga dunia baada, ya kuugua ugonjwa wa saratani tangu mwaka 2019.

Kifo chake kimejiri baada ya kutibiwa nchini Marekani kwa muda mrefu, na kutangaza kuwa amepona ugonjwa huo.

Askofu Kiuna alitangaza amepona ugonjwa wa saratani mwezi Disemba mwaka jana, aliposherehekea miaka 29 katika ndoa na miaka 57 ya kuzaliwa.

Mama Taifa Rachael Ruto na mke wa naibu Rais mchungaji Dorcas Rigathi ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ya kurudisha shukrani.

Wakenya walituma risala za rambirambi kupitia kwa mitandao ya kijamii kwa mke wake Kasisi Kathy Kiuna, watoto wao na familia nzima ya kanisa la JCC.

Afisa mkuu mtendaji wa chama cha hakimiliki za muziki nchini Ezekiel Mutua, alisema Askofu Kiuna atakumbukwa kwa mahubiri yake yaliyobadilisha maisha ya wengi.

“Mahubiri yake yaliwaguza wengi kwa kuwaongezea imani. Alitimiza wajibu wake katika kizazi hiki. Natuma rambirambi zangu kwa kasisi Kathy Kiuna, familia yake na kanisa kwa jumla,” aliomboleza Mutua..

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alitaja kifo cha Askofu Kiuna kuwa pigo kubwa.

“Askofu Allan Kiuna alitekeleza wajibu mkubwa kupitia huduma yake.Mahubiri yake yaliwafaa wengi. Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia yake, marafiki, JCC na kanisa nzima kwa jumla,” alisema Barasa kupitia mtandao wa X.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *