Chama cha Amani National Congress, ANC kimeidhinisha rasmi kujiunga kwake na chama cha United Democratic Alliance, UDA.
Hatua hiyo iliidhinishwa wakati wa mkutano ulioandaliwa katika kaunti ya Lamu Agosti 3, 2024 na kuhudhuriwa na kongozi wa ANC Issa Timamy miongoni mwa viongozi wengine.
Kulingana na Timamy ambaye pia ni Gavana wa Lamu, mkutano huo uliwaleta pamoja zaidi ya wanachama 140 wa ANC wakiwemo wabunge na wawakilishi wadi waliochaguliwa kwa tiketi ya chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
“Taasisi za uongozi wa ANC zimekubaliana na kuazimia kuidhinisha ANC na UDA kuungana kama iivyopendekezwa,” kilisema chama hicho katika taarifa iliyotiwa saini na Timamy.
“Mheshimiwa Gavana Timamy, kiongozi wa chama, amepewa kibali na mamlaka ya kuongoza, kuratibu na kusimamia utekelezaji kamili na uhitimishaji wa ANC na UDA kuungana, suala la muda likiwa muhimu.”
Wakati wa mkutano huo, chama cha ANC ambacho mwasisi wake ni Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi kiliapa kumuunga mkono Rais William Ruto kwa udi na uvumba pamoja na serikali ya Kenya Kwanza.
Rais Ruto ni kiongozi wa chama cha UDA, na hatua ya chama hicho kuungana na ANC inadhamiria kukiimarisha na kukipa sura ya kitaifa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Vyama vingi vya kisiasa humu nchini vimetajwa kuwa vya kikabila, suala ambalo Ruto anafahamika kulipinga akisisiiza umuhimu wa vyama vya kitaifa ili kuupiga dafrau uvundo wa ukabila ambao umekuwa mwiba sugu kwa nchi hii kwa muda mrefu.