Mwanamitindo na mtangazaji wa runinga nchini Marekani Amber Rose amesema kwamba alikuwa anamtania na kumchokoza Beyonce alipodai kwamba alimwibia hotuba yake.
Beyonce alihudhuria na kuhutubia mkutano wa kampeni wa Kamala Harris anayewania urais kupitia chama cha Democratic huko Houston ambapo alifungua hotuba kwa njia ya kipekee.
“Siko hapa kama mtu maarufu, siko hapa kama mwanasiasa, niko hapa kama mama.” alisema mwanamuziki huyo tajika.
Beyonce aliendelea kumpigia debe Harris akisema anaamini uongozi wake utahakikisha nchi bora kwa watoto wote nchini Marekani.
Hotuba ya Beyonce ilichapishwa mitandaoni baadaye na hapo ndipo Rose alitema madai ya Beyonce kumwibia hotuba aliyotoa kwenye mkutano wa kampeni wa Donald Trump anayewania urais kupitia chama cha Republican.
Sasa Amber ameamua kufafanua kuhusu madai yake baada ya kujipata pabaya mitandaoni. Anasema alikuwa akimchokoza na kumtania Beyonce aliyemtaja kuwa rafiki yake.
Alikutana na wanahabari akielekea kuhudhuria sherehe ya Haloween ya Hollywood ambapo alisema anashangaa watu mitandaoni wanamtupia maneno ilhali wake ulikuwa utani tu.
Lakini alisema amejifunza kutokana na tukio hilo na katika siku za usoni atawaza kabla ya kuandika chochote mitandaoni kwani sio kila mtu anapendelea utani.