Bunge la Senate la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limempokonya Rais wa zamani Joseph Kabila kinga yake, na hivyo kutoa nafasi ya Rais huyo wa zamani kufunguliwa mashtaka kwa madai ya kuwaunga mkono waasi mashariki mwa nchi hiyo.
Utawala nchini humo umemshutumu kwa uhaini na uhalifu wa kivita huku ukidai kuwa kuna ushahidi mkubwa unaomhusisha Kabila na kundi la waasi la M23, ambalo limechukua udhibiti wa miji kadhaa mashariki mwa taifa hilo yenye utajiri wa madini.
Kabila mwenye umri wa miaka 53, hajazungumzia shutuma hizo lakini siku za nyuma alikana uhusiano wowote na waasi hao. Takriban maseneta 90 siku ya alhamisi walipiga kura kuunga mkono mashitaka yake ya uhaini, huku watano wakipinga.
Spika wa Seneti Jean-Michel Sama Lukonde alitangaza kwamba seneti imeidhinisha kufunguliwa mashitaka na kuondolewa kwa kinga ya Kabila baada ya kura ya Alhamisi.
Rais huyo wa zamani, ambaye aliongoza nchi hiyo kati ya mwaka wa 2001 na 2019, hakufika mbele ya seneti kujitetea. Baada ya kuachia ngazi, alipewa cheo cha “seneta wa maisha”, ambacho kinampa kinga ya kisheria.
Kabila amekuwa akiishi nje ya nchi, nchini Afrika Kusini, kwa miaka miwili iliyopita. Lakini mwanzoni mwa mwezi uliopita alisema atarejea kusaidia kutafuta suluhu la mzozo huo wa mashariki.