Mwanamuziki wa Uganda Patrick Mulwana maarufu kama Alien Skin ameangaziwa kwa vyombo vya habari kwa sababu ambazo sio za kuridhisha.
Hii ni baada ya mwanamke aitwaye Aisha Namusoke kujitokeza na kudai kwamba Alien ambaye anasema ni mzazi mwenzake aliwahi kumshambulia kabla ya kumpokonya watoto wao watatu.
Namusoke alikuwa akihojiwa ambapo alifichua kwamba yeye ndiye amekuwa mpenzi wa Alien wa muda mrefu, uhusiano wao ukiwa wa muda wa takribani miaka tisa.
Kulingana naye, watoto wao ni wa miaka 7, 5 na miwili unusu.
“Baba ya watoto wangu anaitwa Mulwana Patrick almaarufu Alien Skin, mwanamuziki na niko hapa kusimulia kuhusu matatizo yangu” alisema mwanamke huyo akiongeza kusema kwamba yeye ni mzazi ambaye anadhulumiwa kwa kupigwa nyumbani kwake.
Katika lalama zake, Namusoke alidai kwamba Alien Skin akishirikiana na mpenzi wake mpya aitwaye Namutebi Jowie walimdhulumu mara kadhaa hadi siku moja wakamfurusha kwenye nyumba yake usiku.
Mwanamke huyo sasa anasema anataka haki akiongeza kwamba mateso ya wawili hao dhidi yake sasa yametosha.
“Singefichua haya kwa umma lakini ninapigwa na kukosewa heshima. Wanangu ni wachanga bado siwezi kuwaacha. Alinifukuza nyumbani usiku” alisema.
Naibu msemaji wa polisi wa eneo la jiji la Kampala Luke Owoyesigyire amethibitisha kwamba mwanamke huyo ameripoti kisa chake kwa polisi na uchunguzi umeanzishwa.
Msemaji huyo amesema pia kwamba Alien Skin ameitwa kuandikisha taarifa.