Hatimaye Agnes Kalekye amechukua hatamu kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji, KBC.
Uteuzi wake kwenye wadhifa huo mwezi Mei mwaka huu ulikumbana na visiki kufuatia kesi iliyowasilishwa katika mahakama moja mjini Nakuru.
Karibu miezi sita baadaye, agizo lililomzuia kuanza kuchapa kazi limeondolewa na mahakama na kumruhusu kutekeleza majukumu yake mapya.
“Nimefurahi sana kurejea. Kama mnavyojua, niliteuliwa mwezi Mei lakini kisha kulikuwa na agizo la mahakama. Oktoba 25, mahakama iliondoa agizo hilo na niko hapa. Nimetia saini mkataba wangu na nina shauku ya kuhakikisha shirika hili linafikia upeo wa maendeleo,” alisema Kalekye aliyekaribishwa ofisini na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KBC Tom Mshindi.
“Nitatumia wiki chache zijazo kuzungumza na wafanyakazi kufahamu wanachokifanya kwa sababu naamini tayari kuna mipango. Kwa hivyo, letu sisi ni kufanya tu kazi na wafanyakazi tulio nao kuboresha michakato ya shirika.”
Mshindi alimtakia Mkurugenzi Mkuu huyo mpya wa KBC kila la heri anapochukua hatamu za kuliongoza shirika hilo.
“Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa KBC, ninafuraha ya kumkaribisha Agnes kwa mara nyingine kwa shirika la utangazaji la KBC. Kama unavyokumbuka, ujio wake wakati uliopita ulitatizwa kidogo na agizo la mahakama lakini tuna furaha kwamba agizo hilo sasa limeondolewa,” alisema Mshindi.
“Tunamtakia kila la heri anaposhughulikia masuala mengi ambayo tunajaribu kukabiliana nayo kama shirika. Ni wakati wa mabadiliko, ni wakati wa kulipa shirika hili sura mpya.”
Hadi kufikia wakati Kalekye akichukua usukani wa kuiongoza KBC, Meneja wa Masoko Florence Migunde amekuwa akihudumu kama kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KBC.
Migunde pia amemtakia Kalekye kila la heri katika utendakazi wake kwenye shirika hilo.