Afueni kwa mlanguzi wa mihadarati baada ya kuachiliwa huru na mahakama

Tom Mathinji
2 Min Read
Mlanguzi wa mihadarati Philip Mutune, awachiliwa huru na Mahakama.

Ilikuwa ni furaha isiyo na kifani katika gereza kuu la Thika, baada ya mwanamume aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kwa ulanguzi wa mihadarati ya thamani ya shilingi milioni 5 miaka 10 iliyopita kuachiliwa huru, huku akisubiri kuhitimu kuwa wakili. 

Hatua hiyo ni baada ya yeye kukata rufaa katika mahakama kuu, huku akiachiliwa huru kabla ya kukamilisha kifungo chake.

Safari ya Philip Mutune, ilianza alipokamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata (JKIA) akiwa amebeba mihadarati na kufunguliwa mashtaka katika mahakama za Milimani.

Alizuiliwa katika gereza la viwandani na baadaye kuhamishwa hadi katika gereza kuu la kamiti. Baada ya kuzuiliwa huku kwa muda wa miaka saba, muda alioutaja kuwa mgumu zaidi katika maisha yake, alihamishwa hadi katika gereza la Thika ili kukamilisha kifungo chake.

Kupitia mashirika yasiyo ya serikali kama vile Justice Defenders, ambalo hutoa misaada ya kisheria kuwawezesha wafungwa kupata haki, Mutune alifadhiliwa kusomea sheria.

Alisomea sheria kupitia mtandao katika chuo kikuu cha Strathmore, na anatarajiwa kuhitimu mwezi Disemba.

Philip alianza kutumia ujuzi wake kuwasaidia wafungwa wenzake waliotatizika na aliheshimiwa sana na wafungwa wenzake pamoja na maafisa wa magereza.

Kuhusu kujihusisha kwake na mihadarati, Mutune alisikitikia sana hatua hiyo. “Nilijiunga na watu waovu,lakini jela imenibadilisha,” alisema Mutune.

Alisema anakusudia kuanza upya maisha baada ya kuachiliwa, akilenga kuanzisha kampuni yake ya kutoa huduma za wakili na kuwasaidia wengine katika jamii kujiepusha na makosa.

Afisa msimamizi wa gereza la Thika Hassan Waqo, alimpongeza Mutune akimtaja shupavu, mwenye nidhamu na mtu mwenye maneno machache.

“Kila wakati alikuwa mtulivu na mwenye maono,” aliongeza Waqo.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article