Afua Asantewaa wa Ghana aimba kwa saa 106

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanadada wa taifa la Ghana Afua Asantewaa ameimba kwa muda wa saa 106 akilenga kuvunja rekodi ya dunia ya Guinness ya mtu aliyeimba kwa muda mrefu zaidi.

Asantewaa ambaye ni mwanahabari na mwanabiashara alianza kuimba Jumapili Disemba 24, 2023 usiku wa manane na kufikia leo Disemba 28, 2023 saa tatu asubuhi alikuwa ametimiza muda wa saa 105.

Rekodi ya dunia ya Guinness ya mtu aliyeimba kwa muda mrefu zaidi inashikiliwa na mwimbaji kutoka India Sunil Waghmare na aliiweka mwaka 2012.

Sasa usimamizi wa rekodi za dunia za Guinness unasubiriwa kuthibitisha iwapo Afua ametimiza masharti yote kabla ya kuthibitisha kwamba yeye ndiye mshikilizi mpya wa rekodi hiyo.

Mwanamuziki wa Jamhuri ya Dominican Carlos Silver alikosa kuvunja rekodi hiyo Aprili 2019, hata baada ya kuimba kwa saa 106 kwa sababu ya kutofuata masharti.

Ilibainika kwamba Silver alipumuzika kwa dakika mbili baada ya kila wimbo ilhali muda uliowekwa wa mapumziko ni sekunde 30 kati ya nyimbo.

Matarajio ya Afua kuthibitishiwa rekodi hiyo yako juu kwa sababu alikuwa na kundi la wahudumu ambao walikuwa wanahakikisha kwamba hazidishi muda wa mapumziko kati ya nyimbo.

Aliungwa mkono na wanamuziki tajika waliofika katika eneo la Akwaaba village kumshabikia wakiwemo Shatta Wale, Sista Afia, Sarkodie, Kwabena Kwabena, Efya na Kuami Eugene.

Share This Article