Afrika Kusini, Rwanda kuondolewa kwenye mpango wa AGOA

Serikali ya Marekani tayari imeziarifu Afrika Kusini na Rwanda kuhusu uamuzi huo.

Tom Mathinji
2 Min Read
Donald Trump - Rais wa Marekani.

Afrika Kusini na Rwanda huenda zikaondolewa kwenye mpango wa kibiashara wa Marekani wa AGOA, na hivvyo kupoteza fursa ya kuuza bidhaa nchini humo bila kutozwa ushuru.

Rais Donald Trump amearifu bunge la Marekani kuhusu azma yake ya kuondoa mataifa hayo mawili kwenye mpango huo wa kibiashara kuanzia Januari mosi mwaka 2027.

Mwakilishi wa biashara wa Marekani Jamieson Greer, alisema katika taarifa kwamba uchunguzi wa kila mwaka ulibaini kwamba mataifa hayo husika yalikuwa yakijihusisha katika shughuli zisizoambatana na mahitaji ya mpango huo wa kibiashara.

Kulingana na Greer, serikali ya Marekani tayari imeziarifu Afrika Kusini na Rwanda kuhusu uamuzi huo

Marekani imesema imetekeleza hatua hiyo dhidi ya Afrika Kusini kutokana na wasiwasi kuhusu usalama wa taifa na sera za Mambo ya Nje nchini Afrika Kusini, huku ikiibua wasiwasi nchini Rwanda kuhusiana na hali za kibinadamu, utawala wa sheria na haki za wafanyakazi.

Duru zinaarifu kuwa Afrika Kusini imefaidika zaidi na mpango wa AGOA, ikiuza bidhaa za takriban dola bilioni 1.7 za Marekani mwaka 2025. Baadhi ya bidhaa inazouza Marekani ni pamoja na vipuri vya magari, divai, na matunda ya machungwa.

Mauzo ya Rwanda nchini Marekani yanajumuisha kahawa, chai, na madini.

Hatua hiyo inakuja takribani wiki moja baada ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda kuwekewa vikwazo na Wizara ya Fedha ya Marekani, kutokana na madai ya kuhusika kwake katika uasi wa makundi yenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Share This Article