Afisi ya Mke wa Rais Rachel Ruto kupitia kwa shirika lake la Mama Doing Good inapanga kuandaa hafla za kuinua talanta ya muziki katika kaunti zote 47.
Katika mkutano ulioandaliwa Jumanne Julai 25, 2023 katika Ikulu ya Nairobi, mkewe rais ambaye alikutana na wanamuziki waanzilishi 36, aliahidi pia kuandaa mikutano minne ya kitaifa kuhusu muziki katika muda wa miaka minne ijayo.
Haya yote yatatekelezwa kupitia idara ya talanta katika shirika la Mama Doing Good.
Bi. Rachel alipongeza shirika la hakimiliki ya muziki nchini, MCSK kwa hatua ambazo limechukua ili kuifanya tasnia ya muziki kuwa mchangiaji mkuu katika uchumi wa taifa na katika kutatua matatizo ya mabingwa wa muziki kupitia kwa wakfu wa MCSK.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la MCSK Dr. Ezekiel Mutua alipongeza hatua ya kuandaa mkutano huo wa waanzilishi wa muziki wa injili nchini ambao ni njia moja ya kutambua watu ambao waliweka msingi wa muziki halisi.
Chini ya serikali ya Kenya Kwanza, MCSK imepatiwa leseni ya kuhudumu na viwango vipya vya malipo kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali.
Shirika hilo liko katika harakati za kuhakikisha pesa wanazolipwa waandaaji wa video zinazochapishwa kwenye YouTube zinaongezwa kutoka asilimia 1.7 hadi asilimia 16.5.
Wanamuziki waliohudhuria mkutano wa leo ni Bwana na Bi. Kasanga, Esther Wahome, Munishi, Rose Jeffa, Peace Mulu na Hellen Mtawali kati ya wengine.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kufahamu matatizo yanayokumba sekta ya muziki na kutafuta njia za kuiimarisha kama nguzo muhimu katika uchumi.