Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome ametoa wito kwa wakazi wa sehemu ya Mutuati katika eneo bunge la Igembe Kaskazini, kaunti ya Meru kuwa watulivu huku serikali ikiweka mipango ya kuimarisha usalama.
Hii ni baada ya watu watano kuuawa katika eneo hilo na mamia ya mifugo kuibwa.
Koome aliyezuru sehemu hiyo alisema maafisa wa usalama wanaohudumu katika eneo hilo watakabidhiwa vifaa vya kisasa vya kulinda usalama kuwawezesha kukabiliana na wezi wa mifugo.
Aidha, aliwahimiza wakazi kutolipiza kiasi akisema kuwa wavamihizi hao watatiwa nguvuni.
Kulingana na Koome, ng’ombe wapatao 83 walioibiwa wamepatikana kufuatia msako mkali wa maafisa wa usalama dhidi ya wavamizi hao.
Aliwataka maafisa wa usalama kushirikiana na wakazi hasa wazee wa Njuri Ncheke kwa nia ya kuafikia utangamano wa kijamii.
Jana Jumatatu, majambazi walivamia kijiji cha Njaruine katika eneo la Mutuati na kuwaua watu watano wakiwemo maafisa wawili wa polisi wa akiba kabla ya kuiba mifugo 350.
Kikosi cha maafisa wa polisi wa GSU kimepelekwa katika eneo hilo ili kuimarisha hali ya usalama.