China imesema mabadiliko ya kisiasa nchini Taiwan hayawezi kuzuia juhudi za kufanikisha kile inachokiita “muungano wa kitaifa”.
Haya yanafuatia ushindi mkubwa wa chama tawala cha kisiwa hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Ofisi ya Masuala ya Taiwan ya China ilisema Jumapili kuwa imepokea matokeo ya uchaguzi huo na kuongeza kuwa inaamini maoni ya wananchi wengi nchini Taiwan yanaunga mkono amani, maendeleo na ushirikiano katika Mlango-Bahari wa Taiwan.
Katika taarifa ofisi hiyo ilisema kuwa bila kujali mabadiliko ya hali ya kisiasa ndani ya Taiwan, mwelekeo wa kuimarisha uhusiano na mawasiliano kati ya pande hizo mbili hautabadilika.
Iliongeza kuwa Beijing itaendelea kukabiliana vikali na makundi yanayotaka Taiwan ijitenge na China, kupinga uingiliaji wa mataifa ya nje na kuendeleza juhudi za kufanikisha muungano wa kitaifa.
China inatambua Taiwan inayojitawala kama sehemu ya ardhi yake na haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu ili kukiweka kisiwa hicho chini ya udhibiti wake. Hata hivyo, serikali ya Taiwan inakataa madai ya Beijing kuhusu mamlaka yake juu ya kisiwa hicho.
Baraza la Masuala ya Taiwan huko China Bara limeitaka serikali ya China kukubali matokeo ya uchaguzi wa Taiwan kwa mtazamo wa kiuhalisia na kuanzisha mazungumzo na serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.