Rais Ruto: Tutatekeleza maendeleo kwa usawa

Ruto alisema utawala wake utasambaza rasilimali za kitaifa kwa usawa bila kujali miegemeo ya kisiasa.

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto azindua miradi ya maendeleo Busia.

Rais William Ruto amesema serikali yake imejitolea kuhakikisha maeneo yote ya Kenya yanapokea maendeleo kwa usawa, na kutamatisha miaka ya kutengwa na ukosefu wa maendeleo.

Akiwahutubia wakazi wa Butula, wakati wa ziara yake ya maendeleo katika kaunti ya Busia, kiongozi huyo wa taifa alisema utawala wake utasambaza rasilimali za kitaifa kwa usawa bila kujali miegemeo ya kisiasa.

“Tunaamini maendeleo yenye usawa. kwetu, Usawa ni sawa,” alisema Rais Ruto.

Ruto alitangaza kuwa serikali imewekeza shilingi bilioni 18 kuimarisha miundombinu katika kaunti ya Busia.

Akiwa katika kaunti ya Busia, Rais alikabidhi soko la Bumala kwa wafanyabiashara 320, akisema soko hilo la kisasa lililotumia shilingi milioni 230, lina vifaa vya kuhifadhi chakula, kitovu cha ICT, sehemu za kina mama kuwanyonyesha watoto na vyoo vya kisasa miongoni mwa vifaa vingine.

“Soko hili ni miongoni mwa masoko 17 ya kisasa tunayojenga kote nchini. Tutajenga soko lingine lenye gorofa tatu ili kukidhi idadi kubwa ya wafanyabiashara Bumula,” alisema Rais Ruto.

Pia alitangaza kukamilika kwa mradi wa Lower Nzoia, akisema mifumo yake ya kuzuia maji iliyopanuliwa na kukarabatiwa  itafikisha kikomo tatizo la mafuriko ya muda mrefu  kwenye eneo bunge la Budalang’i huku ikisambaza maji ya unyunyiziaji itakayofanikisha kilimo cha mpunga na mimea mingine.

Aidha, alizindua uwekaji lami wa barabara ya Butula–Nambale–Amukura  na uzinduzi wa miradi ya uunganishaji umeme ya Last Mile  katika maeneo bunge ya Butula, Matayos, na Budalang’i.

Share This Article